Ametoa rai hiyo mkoani Geita alipotembelea mgodi huo kukagua maendeleo ya shughuli za uzalishaji
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameutaka Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef kuhakikisha unatenga kiasi cha dhahabu kwa ajili ya kusafisha kwenye viwanda vya ndani au kuuza katika masoko ya ndani ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo imeanza kununua dhahabu kwa ajili ya akiba.
Ametoa rai hiyo mkoani Geita alipotembelea mgodi huo kukagua maendeleo ya shughuli za uzalishaji pamoja na kuzungumza na kusikiliza changamoto zinazoukabili mradi huo.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa Serikali imeamua kutumia dhahabu inayozalishwa hapa nchini ili kuimarisha akiba ya fedha za kigeni kwa kuhakikisha Benki Kuu ya Tanzania inakuwa na akiba ya dhahabu lakini pia dhahabu inayozalishwa hapa nchini inasafishwa katika Viwanda vya kusafisha madini hayo hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameutaka mgodi huo kusaidia wananchi wanaozunguka mradi huo kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii kujenga miradi endelevu ili hata pale shughuli za uchimbaji zitakapofikia ukomo wakazi hao waendelee kunufaika na miradi hio endelevu.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Gaston Mjwahuzi amesema kuwa Mgodi umepokea maelekezo ya Naibu Waziri Dkt. Kiruswa na kwamba watatekeleza kwa kuwa ni manufaa ya taifa na uchumi kwa ujumla.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Mjwahuzi amesema kuwa hivi sasa mgodi unazalisha wakia tani 1700 hadi 2000 kwa mwezi ambako wanazalisha dhahabu yenye thamani ya shilingi bilioni 8 kwa mwezi.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Geita Kara Magaro ameushukuru mgodi huo kwa kujenga miradi ya huduma za kijamii yakiwemo madarasa na zahanati ambako tangu mradi huo uanze tayari kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 400 zimetolewa na mgodi kama Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) na kusaidia kupunguza adha ya uhaba na uchakavu wa miundombinu katika sekta ya elimu na afya katika Halmashauri hiyo.