Dkt. dugange: ndani ya siku 40 huduma zianze kutolewa kituo cha afya mkoga

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Mhe. Dkt. Festo Dugange ametoa siku 40 kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa kukamilisha na kuanza kutoa huduma katika jengo la wagonjwa nje (OPD) la kituo cha Afya Mkoga kilichopo kata ya Isakalilo.

Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo mkoani Iringa katika ziara yake ya kikazi baada ya kutembelea jengo hilo lililoanza ujenzi mwaka 2021 hadi sasa halijakamilika na shughuli za ujenzi zimesimama huku fedha zaidi ya sh. milioni 130 zikiwa zimetumika katika ujenzi huo kutoka mfuko mkuu wa serikali,Ofisi ya Mbunge na nguvu za wananchi.

“Rais ameleta fedha kwaajili ya wananchi wa Isakalilo waondokane na umbali wakupata matibabu kwenda mjini zaidi ya kilomita 17 na umbali huo unasababisha vifo na akinamama wanafariki kwasababu ya uzembe wa watumishi wa manispaa…sasa wekeni kipaumbele hapa ili ifikapo Januari 30, 2024 tunataka wananchi waanze kupata huduma za OPD hapa,” amesema Dkt. Dugange.

Hata hivyo, Dkt. Dugange amemtaka Mkurugenzi huyo ifikapo Januari 10, 2024 awasilishe taarifa ofisi ya Rais TAMISEMI kuhusu upatikanaji wa fedha za kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.

Aidha, Dkt. Dugange amezitaka Halmashauri zote nchini kuwa na ukomo wa utekelezaji wa miradi na kuepuka kuazisha miradi mipya wakati mingine haijakamilika ili kuepuka matumizi mabaya ya fedha za umma.

Awali, akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Mtendaji wa kata ya Isakalilo, Brison Ngung’ugu amesema kituo hicho kinahitaji sh.milioni 50 kwaajili ya kukamilisha shughuli za ujenzi zilizobaki ikiwamo kufunga milango,kupachika madirisha pamoja na kuweka marumaru.

Share: