Dkt. biteko: jnhpp imeanza kuingiza megawati 235 kwenye gridi ya taifa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa megawati 2,115 umeanza kazi na kuingiza megawati 235 katika gridi ya Taifa kupitia mtambo namba 9.

Hatua hii ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kuwa mtambo huo ungeanza kuzalisha umeme February 25. 2024, ahadi iliyotimizwa siku tatu kabla kuanzia February 22, 2024 mtambo huo ulipoanza uzalishaji.

Dkt. Biteko amesema hayo leo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa baadhi ya Wakuu wa Vyombo vya Habari na Wahariri katika eneo la mradi wilayani Rufiji Mkoani Pwani ambapo wahariri hao walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Bwawa la kuhifadhi maji yatakayozalisha umeme, Tuta Kuu na mitambo ya umeme.

Amesema kuingia kwa megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa kumeboresha hali ya upatikanaji umeme Nchini na kupunguza upungufu wa umeme kwa zaidi ya asilimia 85.

Amesema, utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere unaendelea na ifikapo mwezi March 2024 megawati nyingine 235 zitaingia katika gridi kupitia mtambo namba 8 na kufanya JNHPP kuingiza megawati 470 kwenye gridi na hivyo kupelekea nchi kuwa na ziada ya umeme ya megawati 70.

Share: