TPDC kutokuwa na urasimu katika uchukuaji wa maamuzi mbalimbali ikiwemo kwenye shughuli za utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia ili kutorudisha nyuma sekta hiyo nchini
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuja na mpango wa muda mrefu utakaoonesha jinsi nchi itakavyoweza kuongeza kiasi cha gesi asilia ili muda wote kuwe na hazina ya kutosha ya nishati hiyo inayotumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme, viwandani, majumbani na katika magari.
Dkt. Biteko ameyasema hayo tarehe 21 Novemba, 2023 wakati wa kikao chake na Bodi na Menejimenti ya TPDC ambacho kililenga kufahamiana, kubadilishana mawazo juu ya utendaji kazi na Mhe. Dkt. Doto Biteko kuelekeza matarajio ambayo nchi inayahitaji kutoka TPDC.
Dkt. Biteko pia amewataka TPDC kutokuwa na urasimu katika uchukuaji wa maamuzi mbalimbali ikiwemo kwenye shughuli za utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia ili kutorudisha nyuma sekta hiyo nchini.
Kuhusu maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake, katika Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi na Kijiji cha Madimba na Msimbati mkoani Mtwara, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, maisha ya wananchi katika maeneo hayo ambayo kuna visima na mitambo ya Gesi Asilia lazima yabadilike na wapewe huduma bora ikiwemo maji, umeme, afya na usafiri.