Daraja la mwananchi mwanza kukarabatiwa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff ameagiza Daraja la Mwananchi lililopo Kata ya Mahina jijini Mwanza kuanza kukarabatiwa mara moja kufuatia kuharibiwa na Mvua zinazoendelea kunyesha jijini hapa.

Mhandisi Seff ameyasema hayo jijini Mwanza alipofanya ukaguzi wa miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Mwanza.

Wakati huo huo Mhandisi Seff ameelekeza Km. 4.5 za barabara ya Igongwe-Isanzu-Kabusungu wilaya ya Ilemela ziweke kwenye kipaumbele cha bajeti kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.

Barabara hiyo yenye urefu wa Km. 5.8 inayoelekea hospitali mpya ya Wilaya ya Ilemela ambapo Km. 1.3 zipo kwenye ujenzi wa kiwango cha lami.

Vile vile, Mtendaji Mkuu huyo amewataka Mameneja wa Mikoa wote wa TARURA nchi nzima kufanya ukaguzi wa madaraja na mifereji kabla ya Majira ya mvua kuanza ili kupunguza au kuondoa kabisa madhara na uharibifu wa miundombinu ya barabara pindi mvua zitakaponyesha.

Share: