CAG: Charles Kichere amependekeza Uongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu uweke mwongozo unaohitaji uwasilishaji wa NIDA

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere amependekeza Uongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu uweke mwongozo unaohitaji uwasilishaji wa NIDA kuwa ni lazima kwa Woambaji wote wa mikopo wenye umri wa zaidi ya miaka 18 na Waombaji walio chini ya umri wa miaka 18 wawasilishe watakapofikisha miaka 18 kwa ajili ya kulipwa awamu za mikopo zinazofuata lengo likiwa ni kuimarisha mfumo wa ukusanyaji madeni kwakuwa mfumo wa kutegemea namba za mitihani ya form IV inawafanya washindwe kukusanya madeni kwa Wanafunzi hususani waliojiajiri au kuendelea na masomo zaidi.

Kupitia Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, CAG amesema Bodi pia iwatake Wanafunzi wanaoendelea au wakopaji waliopo kutoa NIDA zao kabla ya kupokea mikopo zaidi na kuingia makubaliano na Wadau wa kimkakati ili kuimarisha ujumuishaji wa mfumo huo hii ni baada ya CAG kubaini Bodi ina deni la mikopo ya Wanafunzi lililoiva la Tsh. trilioni 2.10 hadi tarehe 30 Juni 2023 na imekusanya shilingi trilioni 1.29 (asilimia 62 ya mikopo yote iliyoiva) tangu mwaka 2006/07, hii ikimaanisha kuwa Tsh. trilioni 0.81 (asilimia 38) ya mikopo iliyoiva bado haijakusanywa.

“Ukosefu wa ushirikiano wa mifumo na Wadau wa kimkakati unachangia kushindwa kukusanya mikopo hii, hii inazuia HESLB kutoa mikopo kwa Wanafunzi wengine wenye uhitaji, ukaguzi wangu pia ulipitia utendaji wa urejeshaji mikopo, nilibaini kuwa Bodi haina utambulisho wa lazima na wa kutegemewa wa kipekee kwa Wanafunzi wanaopokea mikopo na kukosa mfumo shirikishi na Wadau wa kimkakati kama utaratibu wa kuwatafuta wanufaika”

“Kwa maoni yangu, kuongezeka kwa idadi ya Wanufaika wa mikopo kunahitaji zaidi kuwa na mfumo thabiti na wa jumla wa utambulisho kama Nambari ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), utekelezaji wa NIDA kama hitaji la lazima utaiwezesha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuwafuatilia wakopaji ipasavyo na kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mikopo, na hatimaye kuhakikisha uendelevu wa utoaji mikopo”

Share: