Benki ya dunia yapongeza rasimu ya dira ya maendeleo ya Tanzania 2050

Nathan Belete, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, ameipongeza serikali ya Tanzania kwa hatua kubwa ilizopiga katika kuandaa rasimu ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Akizungumza Ijumaa, Januari 10, 2025, katika mkutano wa ushirikiano na washirika wa maendeleo wa kuhakiki rasimu hiyo, uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Belete ameelezea kuridhishwa kwake na kazi kubwa iliyofanywa na Wizara husika.

Katika hotuba yake, Belete ameainisha vipengele muhimu ambavyo vinaweza kuboreshwa zaidi ili kuimarisha dira hiyo. Amesisitiza umuhimu wa kuweka msisitizo katika maeneo matano, akianza na hifadhi ya jamii. 

"Uwezo wa nchi kukua kwa njia shirikishi unahusiana moja kwa moja na jinsi hifadhi ya jamii inavyozingatiwa." Hata hivyo, ameangazia changamoto ya kuhakikisha kwamba mifumo ya hifadhi ya kijamii inapata ufadhili endelevu, jambo ambalo linaweza kuwa kikwazo katika utekelezaji wa sera hizo.

Belete pia amegusia mabadiliko ya tabianchi, akipongeza juhudi za serikali za kuingiza suala hilo kwenye dira ya maendeleo.

"Mabadiliko ya tabianchi hayapaswi kushughulikiwa tu katika sekta chache za uzalishaji, bali inapaswa kuzingatiwa katika kila sekta." Aliongeza kuwa mikakati bora ya kushughulikia changamoto za tabianchi ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Aidha, alitoa changamoto kwa serikali kuzingatia nafasi ya Tanzania katika ushirikiano wa kikanda, akisema kwamba hili ni eneo lenye fursa kubwa. "Suala la ushirikiano wa kikanda, hasa kwenye vipengele vya biashara, linapaswa kupewa kipaumbele zaidi na kuendana na mpango wa uwekezaji wa umma”.

Share: