Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia (WB) wamesaini mikataba miwili yenye thamani ya dola za Marekani milioni 104, sawa na takriban shilingi bilioni 248, kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Nchini Tanzania maarufu kama “PAMOJA”.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika Jijini Dar es salaam kati ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa niaba ya Serikali na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete.
Akifafanua kuhusu mikataba hiyo, Dkt. Nchemba amesema kuwa mkataba wa dola za Marekani milioni 4, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 9.5 ni msaada na mkataba wa dola za Marekani milioni 100, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 238 ni mkopo wenye masharti nafuu.
Amesema mradi wa PAMOJA uliosainiwa utasaidia kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi kwa Wanawake pamoja na huduma za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia Tanzania Bara na Zanzibar “Hili litatimizwa kupitia uimarishaji vikundi vya wanawake kwa kuwajengea ujuzi wa biashara na kuwaunganisha na fursa za masoko, kuongeza fursa za mikopo nafuu kwa vikundi vya wanawake, kuwaongezea upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia mifumo rasmi ya kifedha pamoja na kuimarisha huduma za kukabiliana na ukatili wa kijinsia”
Amesema mradi huo utawanufaisha moja kwa moja Wanawake wapatao 319,850 na walengwa wengine 399,000, wakiwemo Wanafamilia za wanufaika.