Bei kubwa za dawa nigeria kumewafanya baadhi ya wagonjwa kugeukia tiba ya asili

Gharama za kubwa za baadhi ya dawa nchini Nigeria kiwango ambacho kimepanda takribani mara kumi katika miezi michache iliyopita, kimewalazimisha baadhi ya wagonjwa kupunguza dozi au kugeukia tiba asilia.

Maafisa wa sekta ya dawa wamesema kushuka kwa thamani ya Naira baada ya kuondolewa katika udhibiti wa sarafu mwezi Juni kumefanya bei za bidhaa mpya kupanda.

Wakati Sodiq Ajibade alipokuwa akitoka katika duka la dawa mjini Lagos alikuwa ameshika dawa za pumu, aina moja ya dawa hakuwa nayo mkononi mwake kwa sababu hana pesa za kuinunua.

“Nilikuwa nikinunua dawa nilizoandikiwa na daktari za aina tatu, lakini sasa nimepunguza na kununua mbili ambazo ni penicillin na aminophylline” alisema Ajibade.

Rais wa Jumuiya ya Famasia ya Nigeria Cyril Usifoh, amesema dawa nyingi zinatoka nje ya nchi wakati watengenezaji wa ndani wanategemea uagizaji wa malighafi za kutengenezea dawa kutoka nje.

Tangu mwezi Juni, Naira imepoteza nusu ya thamani yake, na kuongeza bei ya kila kitu kuanzia dawa za maumivu mpaka dawa za magonjwa sugu.

Waziri wa Afya wa Nigeria na Shirika la Taifa la Chakula pamoja na Utawala na Udhibiti wa dawa haukuweza kujibu maombi ya maoni.

Msemaji wa GSK amesema uhaba wa fedha za kigeni umeathiri uwezo wa GSK kusambaza dawa na chanjo katika masoko, na kusababisha kutoweka kwa dawa madukani.

Share: