Mtendaji Mkuu nataka kuona jitihada yenu katika ukusanyaji wa madeni yote mnayodai, hakikisheni madeni yanalipwa kwa wakati.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuongeza bidii ya ukusanyaji wa madeni kwa wapangaji wao na kuweka mikakati itakayowawezesha kukusanya madeni hayo ili kupata fedha za kujenga nyumba nyingine za kisasa na kuwezesha watumishi wengi wa umma kupata huduma ya nyumba na makazi bora.
Hatua hiyo inafuatia kutoridhishwa na kasi ya ukusanyaji madeni iliyopo sasa katika majengo yake nchini kote.
Akizungumza katika kikao kazi na Menejimenti ya TBA, Waziri huyo ameutaka Wakala huo kuandaa kanzi data ya majengo yote inayoyamiliki na viwanja nchini kote ili kuisimamia kikamilifu na hivyo kuwawezesha kuja thamani ya mali iliyopo.
“Mtendaji Mkuu nataka kuona jitihada yenu katika ukusanyaji wa madeni yote mnayodai, hakikisheni madeni yanalipwa kwa wakati bila kujali nani anayedaiwa, amesema Bashungwa.
Waziri Bashungwa ameagiza Wakala huo kuhakikisha mtazamo uliopo makao makuu ya TBA katika kukusanya madeni, kubuni miradi mipya ya kisasa na kuwaelimisha watumishi uwepo katika mikoa yote ili miradi ya ujenzi wa kisasa ifanyike na kodi zikusanywe kikamilifu na kuipa TBA hadhi inayostahili.