Africa 50 - afdb kusaidia ujenzi wa bandari shirikishi zanzibar

Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo yote muhimu ya uwekezaji wa miundombinu ili kuiwezesha nchi kuwa na ukuaji endelevu wa kiuchumi,

Serikali ya Tanzania na Taasisi ya Uwekezaji wa Miundombinu Afrika (Africa 50) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), wamekubaliana kuendeleza huduma za bandari Visiwani Zanzibar.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, katika kikao kati ya Tanzania na Taasisi hiyo kilichofanyika kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jijini Nairobi nchini Kenya.


Dkt. Akili alisema Serikali imekubaliana kuendeleza mazungumzo ambayo yalishaanza kufanyika na Taasisi ya Uwekezaji wa Miundombinu Afrika (Africa 50) kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Shirikishi ya Manga Pwani na Taasisi hiyo pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wanatarajia kufika Zanzibar mwezi Juni, 2024 kuangalia eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo.

“Tunatarajia hivi karibuni, Africa 50 kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), watakuja Zanzibar kwa ajili ya kuangalia eneo lilioandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Manga Pwani”, alibainisha Dkt. Akil.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil Aliongeza kuwa Africa50 pia imeahidi kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kuhakikisha mradi huo unakamilika mapema ili uweze kusaidia kuhamasisha uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

Aidha,Dkt. Akil alisema kuwa, tofauti na mradi huo wa ujenzi wa Bandari ya Manga pwani Taasisi ya Uwekezaji wa Miundombinu Afrika (Africa50) imekuwa ikishirikiana na Serikali katika maeneo mbalimbali ya maendeleo hususan katika Sekta ya Nishati upande wa gesi ambapo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC).


Kwa upande wake Mkuu wa Uendeshaji wa Taasisi ya Uwekezaji wa Miundombinu Afrika (Africa 50), Bi. Tshepidi Moremong, alisema Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo yote muhimu ya uwekezaji wa miundombinu ili kuiwezesha nchi kuwa na ukuaji endelevu wa kiuchumi, kuzalisha ajira na kutunza rasilimali za asili kwa vizazi vijavyo.

Alisema Taasisi hiyo inachangia ukuaji wa nchi za Afrika kwa kuleta pamoja miradi ya maendeleo na ufadhili katika jukwaa moja, inaendeleza na kuwekeza katika miradi inayoweza kufadhiliwa, kuchochea mtaji wa Sekta ya Umma na kuhamasisha ufadhili wa Sekta Binafsi.

Africa50 ilianzishwa na Serikali za Afrika kwa pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ili kusaidia kuziba pengo la ufadhili wa miundombinu Barani Afrika kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kuchochea upatikanaji wa fedha ili kuendeleza Sekta ya Umma na Binafsi, pamoja na kuwekeza katika maeneo ya miundombinu Barani Afrika.

Share: