Mfanyabishara singida akamatwa kwa kuuza sukari bei ambayo sio elekezi

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amefanya ziara ya kushtukiza na kubaini Wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei kubwa ambapo amefanikisha kukamatwa kwa Mfanyabiashara mmoja aliyekutwa akiuza mfuko wa kilo hamsini kwa Tsh. 189,000 tofauti na bei elekezi ya Tsh. 140,000 hadi Tsh. 145,000 kwa bei ya jumla.

Gari moja lenye shehena ya sukari lilionekana wakati msafara wa Mkuu huyo wa Mkoa ukipita katikati ya Mji wa Manyoni ambapo baada ya kuulizwa walidai wamenunua kwenye duka la Mfanyabiashara huyo waliyemtaja kuwa ni Mayengela Mboji.

Baada ya maelezo ya Wateja hao RC Serukamba aliyeambatana na kamati ya Usalama Wilaya ya Manyoni, waliingia katika duka hilo na kukagua risiti za mauzo ambapo ikabainika Mfanyabiashara huyo anauzia Wateja sukari hiyo kwa kati ya shilingi 184,000 na 189,000 kwa mfuko wenye ujazo wa kilo 50.

Itakumbukwa February 21,2024 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa aliwaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini kusimamia kwa makini usambazaji wa sukari na kuwachukulia hatua Wafanyabiashara wote wanaohujumu upatikanaji wake

Share: