ANAYEDAIWA KUWA KIONGOZI WA MTANDAO WA UKAHABA DUBAI AKAMATWA

Charles Mwesigwa, anayejulikana zaidi kwa jina la “Abbey,” anayedaiwa kuwa kinara wa genge la biashara haramu ya kuwauza wanawake kingono nchini Dubai, amekamatwa na polisi baada ya kuwekwa wazi kupitia uchunguzi wa BBC.

Kwa mujibu wa taarifa, tahadhari ya hatari iliyotolewa na Interpol kupitia mamlaka za Uganda ndiyo iliyowezesha polisi wa Dubai kumtia mbaroni.

Uchunguzi uliofanywa na BBC umebaini kuwa Abbey alikuwa akihadaa wasichana kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Uganda, kwa ahadi za ajira zenye staha. Hata hivyo, walipofika Dubai walijikuta wakiangukia kwenye mtego wa mtandao wa biashara ya ngono.

Makala hiyo imeonesha kuwa wanawake walikuwa wakiuzwa kingono kwa bei ya kuanzia Dola za Marekani 1,000 (takribani Shilingi milioni 2.5 za Kitanzania), mara nyingi kwa sherehe binafsi za matajiri. Aidha, uchunguzi huo umebainisha kwamba baadhi ya wateja walihusisha vitendo vya unyanyasaji wa kupindukia, ikiwemo kuwalazimisha wasichana hao kushiriki katika matendo ya kudhalilisha kwa malipo ya ziada huku wakirekodiwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ukatili huo uliwafanya angalau wasichana wawili kujitoa uhai kutokana na madhila waliyopitia.

Kukamatwa kwa Abbey kunatazamiwa kuwa hatua muhimu katika kupunguza mtandao huu wa kikatili unaoendelea kulalamikiwa kwa kuathiri maisha ya wanawake vijana hususan kutoka Afrika Mashariki

Share: