
Familia za abiria wanne waliofariki kwenye ndege ya Air India iliyoanguka mwezi Juni wamewasilisha kesi nchini Marekani dhidi ya kampuni ya ndege ya Boeing na kampuni ya kutengeneza vipuri vya ndege ya Honeywell, wakizituhumu kampuni hizo kwa uzembe.
Kesi hiyo iliyowasilishwa Jumanne, na iliyoonekana na BBC, ilisema swichi zenye hitilafu za mafuta zilisababisha ajali hiyo na kuzishutumu kampuni hizo kwa "kutofanya lolote" licha ya kufahamu hatari za muundo wa ndege hiyo.
Ndege ya Air India 171 iliyokuwa ikielekea London Gatwick, Boeing 787, ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka Ahmedabad na kuua watu 260.
Swichi za mafuta zimekuwa angalizo kwa wachunguzi baada ya uchunguzi wa awali kubaini kuwa mafuta kwa injini yalikatika muda mfupi baada ya ndege kupaa.