
Umoja wa Falme za Kiarabu umeionya Israel kwamba kutwaa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu " kutavuka mpaka" na kudhoofisha ari ya Mkataba wa Abraham ambao ulirejesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Afisa mkuu wa Imarati, Lana Nusseibeh, alisema hatua hiyo itakuwa mwisho wa kutafuta suluhisho kwa mataifa hayo mawili katika mzozo wa Israel na Palestina.
Wizara ya mambo ya nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imesema inakaribisha msimamo wa UAE.
Serikali ya Israel haijatoa maoni yoyote. Lakini matamshi ya Nusseibeh yalikuja baada ya Waziri wa Fedha mwenye msimamo mkali Bezalel Smotrich kufichua pendekezo la kutwaliwa kwa takriban theluthi nne za Ukingo wa Magharibi.
Israel imejenga takriban makazi 160 ya Wayahudi 700,000 tangu ilipoikalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki - ardhi ambayo Wapalestina wanataka, pamoja na Gaza, kwa taifa linalotarajiwa - wakati wa vita vya Mashariki ya Kati vya 1967. Takriban Wapalestina milioni 3.3 wanaishi kando ya eneo hilo..
Makazi hayo ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa.