
Rais wa Colombia, Gustavo Petro, amelaani mashambulizi ya anga yanayofanywa na Marekani dhidi ya boti zinazoshukiwa kusafirisha dawa za kulevya katika Bahari ya Karibea, akiyaita kuwa ni “kitendo cha dhuluma.”
Katika mahojiano na BBC, Petro alisisitiza kuwa iwapo itathibitika kuwa raia wa Colombia waliuawa kwenye operesheni hizo, maafisa wa Marekani wanaohusika wanapaswa kufikishwa mahakamani na kujibu mashtaka ya jinai.
Mashambulizi hayo, ambayo yameripotiwa kusababisha vifo vya watu 17 tangu kuanza kwake mwezi huu, yametajwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kama hatua ya kukabiliana na ulanguzi wa fentanyl na dawa nyingine haramu zinazoingia nchini humo.
Hata hivyo, wachambuzi wa sheria na baadhi ya wabunge wameibua wasiwasi kuhusu uhalali wa operesheni hizo chini ya sheria za kimataifa na haki za binadamu.
“Kwa nini utumie makombora wakati unaweza kusimamisha boti na kuwakamata wafanyakazi wake?” alihoji Petro. “Vinginevyo, hayo ni mauaji.”
Akiendelea kuzungumza na BBC Jumatano, Petro alisema jitihada za kupambana na mihadarati hazipaswi kugeuka operesheni za kijeshi zinazohatarisha maisha ya watu, akisisitiza kwamba “watu wasiuawa” kwa kisingizio cha vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya.