TRUMP ADAI HUJUMA TATU WAKATI WA MKUTANO WA UMOJA WA MATAIFA

Rais wa Marekani, Donald Trump, ametaka kufanyika kwa uchunguzi wa haraka kuhusu matukio aliyoyaita “hujuma tatu” yaliyotokea wakati wa ziara yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano.

Kupitia ujumbe kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump alitaja tukio la ngazi ya umeme kukwama wakati akiwa na mkewe Melania, kuharibika kwa kifaa alichotumia kusoma hotuba yake, na changamoto za kusikika ukumbini kama ishara za makusudi ya kumharibia.


Afisa wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa mfumo wa sauti uliotumika katika ukumbi huo uliundwa mahsusi kurahisisha watu kusikia tafsiri kupitia visikizi.


Hata hivyo, Trump alisisitiza kuwa matukio hayo hayakuwa ajali za kawaida. “Kilichotokea jana katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa ni FEDHEHA – si mara moja, wala mbili, bali mara tatu!” aliandika. “Hii haikuwa bahati mbaya, bali hujuma ya wazi ndani ya Umoja wa Mataifa. Wanapaswa kuona haya.”


Trump pia alisema atamuandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akisisitiza umuhimu wa kufanyika uchunguzi na hatua kali kuchukuliwa. Aliitaka pia mifumo ya usalama, ikiwemo kamera kwenye sehemu ya ngazi, ichunguzwe hasa katika eneo la kitufe cha dharura kinachoweza kusimamisha ngazi.


Akirejea taarifa ya gazeti la Times lililoripoti kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walitania kuhusu kuzima ngazi, Trump alidai kitendo hicho kilikuwa “hujuma ya wazi” na akasisitiza watu waliohusika wakamatwe.


Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, ameunga mkono wito wa rais, akisema matukio hayo “hayakubaliki kabisa” na yanapaswa kuchunguzwa rasmi.

Share: