AKUTWA  NA HATIA YA NJAMA YA KUMUUA DONALD TRUMP

Ryan Routh, mwenye umri wa miaka 59, amehukumiwa kwa kosa la kujaribu kumuua Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, katika tukio lililotokea kwenye uwanja wa gofu huko Florida mwezi Septemba mwaka jana.

Kwa mujibu wa mahakama, Routh alipatikana na hatia katika mashtaka yote yaliyowasilishwa, yakiwemo jaribio la mauaji dhidi ya mgombea mkuu wa urais na makosa kadhaa yanayohusiana na matumizi ya silaha.

Tukio hilo lilijiri tarehe 15 Septemba 2024, wakati Trump, ambaye wakati huo alikuwa akigombea tena urais, akicheza gofu katika uwanja ulioko ufukweni mwa West Palm Beach, karibu na makaazi yake ya Mar-a-Lago.

Mara baada ya hukumu kutangazwa, Routh alijaribu kujidhuru kwa kutumia kalamu kama kisu, lakini askari wa Marekani waliokuwa mahakamani waliingilia kati na kumzuia, taarifa za vyombo vya habari vya Marekani zilisema.

Katika ujumbe aliouweka kwenye mitandao ya kijamii baada ya hukumu, Trump aliwashukuru maafisa wa usalama pamoja na shahidi aliyetoa taarifa zilizosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa. "Alikuwa mtu hatari mwenye nia ovu, lakini walimkamata. Ni ushindi mkubwa kwa haki nchini Marekani!" aliandika Trump.

Mwanasheria mkuu wa serikali, Pamela Bondi, naye alilaani kitendo hicho, akisema: “Jaribio hili la mauaji halikuwa shambulio tu kwa rais wetu, bali pia ni fedheha kwa taifa lote.”

Share: