DRC NA RWANDA ZAKUBALIANA KUANZA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA AMANI

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda zimetangaza kuanza kutekeleza hatua za kiusalama chini ya makubaliano ya upatanishi yaliyosimamiwa na Marekani, kuanzia mwezi ujao. Hatua hii inachukuliwa kama hatua muhimu katika safari ya kuelekea amani, licha ya hofu iliyokuwepo kuhusu kuchelewa kwa utekelezaji.

Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao kilichofanyika Washington mnamo Septemba 17–18, na taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatano ilithibitisha kwamba utekelezaji utaanza rasmi Oktoba 1. Taarifa hiyo pia iliungwa mkono na Marekani, Qatar, Togo pamoja na Kamisheni ya Umoja wa Afrika.


Kwa mujibu wa vyanzo vilivyonukuliwa na shirika la habari la Reuters, hatua hizo za kiusalama zinatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu. Operesheni kuu zitahusisha kuondoa tishio la kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), lenye makao makuu mashariki mwa Congo, sambamba na kuondolewa kwa wanajeshi wa Rwanda waliopo nchini humo. Vyanzo hivyo vinasema shughuli hizo zimepangwa kufanyika kati ya Oktoba 21 na 31.


Mpango huo sasa unatoa ratiba ya wazi ya namna Rwanda na DRC zitakavyotekeleza makubaliano hayo ya amani, jambo lililokuwa likikosekana awali.


Mawaziri wa mambo ya nje wa Congo na Rwanda walitia saini mkataba huo Juni 27 mjini Washington, na siku hiyo hiyo walikutana na Rais wa Marekani, Donald Trump. Marekani imedokeza kuwa inatarajia makubaliano haya yaende sambamba na kuvutia mabilioni ya dola za uwekezaji kutoka nchi za Magharibi katika ukanda huo wenye utajiri mkubwa wa madini kama tantalum, dhahabu, kobalti, shaba na lithiamu.

Share: