Halijoto huko Mekka ilipanda hadi 51.8C, kulingana na kituo cha kitaifa cha hali ya hewa cha Saudi Arabia.
Takriban watu 1,301 walikufa wakati wa Hijja, Saudi Arabia inasema, wengi wao wakiwa mahujaji ambao hawakuidhinishwa waliotembea, umbali mrefu kwenye joto kali.
Hijja ya mwaka huu ilifanyika wakati wa wimbi la joto, joto wakati mwingine linazidi nyuzi joto 50 (122F).
Zaidi ya robo tatu ya waliofariki hawakuwa na vibali rasmi vya kuwa huko na walitembea chini ya jua moja kwa moja bila makazi ya kutosha, shirika rasmi la habari la Saudi SPA lilisema.
Baadhi ya waliofariki walikuwa wazee au wagonjwa, shirika hilo liliongeza.
Waziri wa Afya Fahd Al-Jalajel alisema juhudi zimefanywa ili kuwahamasisha watu juu ya hatari ya shinikizo la joto na jinsi mahujaji wanaweza kukabiliana na hali hiyo.
Vituo vya afya viliwahudumia karibu mahujaji nusu milioni, wakiwemo zaidi ya 140,000 ambao hawakuwa na kibali, alisema, na wengine bado wako hospitalini kutokana na athari ya joto.
"Mwenyezi Mungu awasamehe na kuwarehemu marehemu. Rambirambi zetu ziende kwa familia zao," alisema.
Saudi Arabia imekosolewa kwa kutofanya juhudi ya kutosha kuhakikisha Hija inakuwa salama zaidi, haswa kwa mahujaji ambao hawajasajiliwa ambao hawana huduma kama vile mahema yenye viyoyozi na usafiri rasmi wa Hija.
Halijoto huko Mekka ilipanda hadi 51.8C, kulingana na kituo cha kitaifa cha hali ya hewa cha Saudi Arabia.
Mataifa tofauti duniani yamekuwa yakitoa maelezo juu ya idadi ya raia wao waliofariki, lakini Saudi Arabia haikuwa imetoa kauli yoyote hadharani juu ya vifo hivyo au kutoa idadi rasmi hadi Jumapili.
Shirika la habari la AFP lilimnukuu mwanadiplomasia wa Kiarabu akisema Wamisri 658 wamefariki. Indonesia ilisema zaidi ya raia wake 200 walipoteza maisha, huku India ikitoa idadi ya vifo vya watu 98.
Pakistan, Malaysia, Jordan, Iran, Senegal, Sudan na eneo linalojiendesha la Kurdistan la Iraq pia zimethibitisha vifo.