Serikali ya malawi inasema israel imewatimua wafanyakazi 12 wa malawi waliokuwa wameajiriwa

Raia hao 12 wa Malawi walikuwa miongoni mwa wafanyakazi zaidi ya 40 wa kigeni waliokamatwa wakifanya kazi katika kiwanda cha kuoka mikate huko Tel Aviv

Serikali ya Malawi inasema Israel imewatimua wafanyakazi 12 wa Malawi waliokuwa wameajiriwa kufanya kazi katika mashamba maalum nchini humo.

Katika taarifa, Waziri wa Habari Moses Kunkuyu alisema wafanyikazi hao walikuwa na visa halali ya kufanya kazi katika mashamba maalum lakini "wamekiuka kandarasi yao" kwa kwenda kufanya kazi katika duka la mikate.

Raia hao 12 wa Malawi walikuwa miongoni mwa wafanyakazi zaidi ya 40 wa kigeni waliokamatwa wakifanya kazi katika kiwanda cha kuoka mikate huko Tel Aviv wiki iliyopita.

Bw Kunkuyu alisema ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za Israel kwa mfanyakazi wa kigeni kubadilisha kazi bila kufuata taratibu zinazofaa.

Aliwaonya wafanyakazi wote wahamiaji wa Malawi nchini Israel "kuachana na tabia kama hiyo kwani inaiweka nchi hii katika sifa mbaya".

"Tabia kama hiyo inaweza pia kupunguza nafasi za ajira za watu husika," alisema. Mamia ya Wamalawi walisafiri hadi Israel mwaka jana ili kuziba pengo la wafanyakazi katika mashamba ya Israel, kwani maelfu ya wafanyakazi walikuwa wameondoka kufuatia kuanza kwa vita na Hamas mwezi Oktoba.

Ilikuja kama sehemu ya mkataba wa mauzo ya wafanyikazi uliotiwa saini kati ya nchi hizo mbili mnamo 2022.

Wiki iliyopita, baadhi ya Wamalawi Israel waliambia BBC kwamba mishahara duni ndiyo iliyowafanya baadhi yao kuacha kazi zao kwenye mashamba na kutafuta kazi nyingine nchini humo.

Share: