Marekani iliitaka Israel iwatambue hadharani wapiganaji wa Hamas iliosema wamewaua
Marekani imeiambia Israel ni lazima iwe wazi kabisa kuhusu shambulizi la anga ambalo limeripotiwa kuua takriban watu 35 katika shule ya kati ya Gaza iliyojaa watu waliokimbia makazi yao Alhamisi asubuhi.
Waandishi wa habari wa eneo hilo waliambia BBC kuwa ndege ya kivita ilikuwa imerusha makombora mawili kwenye madarasa kwenye ghorofa ya juu ya shule katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat mjini.
Jeshi la Israel lilisema lilifanya shambulizi "sahihi" kwenye "kiwanja cha Hamas" katika shule hiyo, lakini ofisi ya vyombo vya habari vya serikali ya Gaza inayoongozwa na Hamas ilikanusha madai hayo.
Marekani iliitaka Israel iwatambue hadharani wapiganaji wa Hamas iliosema wamewaua - sawa na vile jeshi la Israel lilivyotoa majina tisa kati yao.
Israel mara nyingi huwatambua wanamgambo inaowalenga katika mashambulizi ya anga lakini ni nadra kwa Marekani kuihimiza kufanya hivyo.
Waisraeli "walituambia kuna wanamgambo 20 hadi 30 waliokuwa wakiwalenga [na] watatoa majina ya wale wanaoamini kuwa wamewaua, wapiganaji hao", msemaji wa idara ya serikali ya Marekani Matthew Miller alisema.
“Hicho ndicho wamesema watatoa. Tunatarajia watafanya hivyo, pamoja na maelezo mengine yoyote ambayo yatatoa mwanga juu ya tukio hili."
Katika taarifa ya habari iliyokaribia kwa wakati mmoja, msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alitoa majina ya wapiganaji tisa wa Hamas na Islamic Jihad aliosema wameuawa katika shambulizi hilo. Alisema zaidi watatambuliwa baada ya "kuthibitisha taarifa".
Mjini Washington, Bw Miller alisema Marekani imeona ripoti kwamba watoto 14 waliuawa katika shambulizi hilo.
"Ikiwa ni kweli kwamba watoto 14 waliuawa, hao sio magaidi," alisema.
"Na kwa hivyo serikali ya Israel imesema itatoa taarifa zaidi juu ya shambulizi hili... Tunatarajia watakuwa wawazi kabisa katika kuweka taarifa hizo hadharani."
Vifo vya hivi punde vimetokea wiki moja tu baada ya watu 45 kuuawa katika shambulio la Israel katika mji wa Rafah huko Gaza.