Maafisa wa congo wakanusha kuhusu kufanya mazungumzo na maafisa wa israel juu ya makazi mapya ya palestina

Maafisa wa Congo kutoka upande wa Kinshasa na Brazzaville wamekanusha ripoti kwamba wakimbizi wa Kipalestina watapewa makazi mapya Afrika ya kati kama sehemu ya makubaliano na Israel.

Gazeti la The Times of Israel mapema wiki hii liliripoti kwamba Serikali ya Muungano ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa katika "mazungumzo ya siri" na Jamhuri ya Kongo ili kuwapa makazi maelfu ya watu kutoka Gaza.

Ilinukuu chanzo katika baraza la mawaziri la usalama ambaye inasemekana alisema Kongo ilikuwa "tayari kuwapokea wahamiaji".

Hata hivyo, msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kongo na Waziri wa Mawasiliano na Vyombo vya Habari, Thierry Moungalla alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba nchi hiyo haijafanya mazungumzo na Israel kuhusu kuwapokea wahamiaji kutoka Gaza.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Vyombo vya Habari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Patrick Muyaya, alisema katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii wa X: “Kinyume na inavyoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari, hakujakuwa na aina yoyote ya mazungumzo, majadiliano au mpango kati ya serikali yetu na serikali ya Israel kuhusu madai ya kupokea wahamiaji wa Kipalestina katika ardhi ya Kongo.

Mapema wiki hii Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, mwanachama wa Chama cha Kidini cha Kizayuni chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia alitoa wito kwa karibu Wapalestina wote wa Gaza kuondoka kwenye ukanda huo kupitia mpango wa "uhamiaji" ili kutoa nafasi kwa walowezi wa Israel.

Waziri wa usalama wa taifa wa Israel Itamar Ben-Gvir, wa chama chenye siasa kali za mrengo wa kulia, Otzma Yehudit (Jewish Power) pia alisema Israel inapaswa "kuwahimiza wakazi wa Gaza kuhama".

Josep Borrell Fontelles, Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya wa Masuala ya Kigeni na Sera ya Usalama alielezea kauli hiyo kama "ya uchochezi na kutojali" katika taarifa kwenye mtando wa X. "Uhamisho wa kulazimishwa ni marufuku na ni ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya haki za kibinadamu," aliongeza.

Wakati msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matthew Miller alisema: "Gaza ni ardhi ya Wapalestina na itasalia kuwa ardhi ya Palestina, na Hamas haidhibiti tena mustakabali wake na hakuna makundi ya kigaidi yanayoweza kutishia Israel."

Katika kipindi cha miezi michache iliyopita serikali ya Israel imeendeleza mipango ya karibu makazi mapya 5,700 katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, licha ya shinikizo la Marekani kusitisha upanuzi wa makazi hayo.

Zaidi ya Wapalestina 22,000 - wengi wao raia - wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu vita kuanza kwa vita, kulingana na wizara ya afya ya Gaza ambayo inaendeshwa na kundi la Hamas.

Israel yalianza mashambulizi ya kulipiza kisasi baada ya wanamgambo wa Hamas kufanya shambulio la kushtukiza kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, na kuua watu 1,200 na kuwateka nyara watu 240.

Share: