anajulikana sana kwa jengo lake lililo katikati ya jiji la Kigali ambalo lilijulikana kama UTC
Bilionea wa Rwanda Tribert Rujugiro Ayabatwa, ambaye alikuwa amekimbia Rwanda kwa miaka mingi, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 83.
Wakati huo katika mahojiano na gazeti la New Vision la nchini Uganda la mwaka 2019, alisema kuwa hajui umri wake kamili kwa sababu wakati alipozaliwa hakukuwa na njia ya serikali kurekodi watoto waliozaliwa, ila kaambiwa kuwa alizaliwa mwanzoni mwa miaka ya 1940.
Mmoja wa mawakili wake aliongelea kuhusu kifo cha Rujugiro, na kuongeza: "Hatuna taarifa zaidi za kutoa kwa sasa."
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, alikuwa akiishi Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Rujugiro alikuwa mmoja wa wafadhili muhimu wa Rwanda ambaye aliwasaidia kifedha waasi wa RPF-Inkotanyi katika vita walivyopigana na Jeshi la Rwanda (FAR) enzi hizo kuanzia tarehe mosi Oktoba mwaka 1990, hadi RPF ilipotwaa madaraka Julai mwaka 1994.
Mnamo mwaka wa 2014, jarida la Forbes lilitangaza kuwa Rujugiro ndiye mfanyabiashara tajiri zaidi wa tumbaku barani Afrika.
Kabla ya kutofautiana na serikali ya Rwanda na kukimbilia Afrika Kusini mwaka 2010, alikua mshauri wa Rais wa Rwanda Paul Kagame.
Nchini Rwanda, Rujugiro anajulikana sana kwa jengo lake lililo katikati ya jiji la Kigali ambalo lilijulikana kama UTC (Union Trade Centre), ambalo ni moja ya majengo ya kwanza kujengwa baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.
Jengo hilo linakadiriwa kuwa na thamani ya takriban dola za kimarekani milioni 20
Lilifungua milango yake mnamo 2006.Serikali ilipiga mnada jengo hilo mwaka 2017 ikidai kuwa Rujugiro, mwenye hisa nyingi, anadaiwa kodi ya zaidi ya dola milioni moja, jambo ambalo ameendelea kukanusha.
Wakati jengo hilo likipigwa mnada, tayari kulikuwa na kesi kati ya Rujugiro na serikali ya Rwanda katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kuhusu uvamizi wa jengo hili mwaka 2013 na wilaya ya Nyarugenge kwa madai kuwa ‘’mali isiyo na wamiliki’’.
Mnamo Agosti 2022, mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini Arusha, Tanzania, iliamuru serikali ya Rwanda imlipe Rujugiro fidia ya dola milioni moja kwa sababu ya kudhibiti na kuuza jengo hilo kinyume cha sheria.
Wakati huo, baada ya uamuzi wa mahakama katika rufaa hiyo, Rujugiro aliiambia BBC kwamba kwake pesa hizo zilitosha, "kwa sababu kilichonipeleka huko mahakamani sio wao kunipa fidia kilichonipeleka pale ni kutaka warudishe jengo langu."
Alipoulizwa iwapo jengo hilo halitarejeshwa kwake ataendelea kushtaki, alijibu: "Hapana, hatutabishana, nitasubiri, kwa sababu wanasema kwamba hakuna mvua inayonyesha daima.
"Naweza kusubiri serikali hiyo iondoke, na nyingine itanirudishia".
Rujugiro pia amekuwa maarufu nchini Burundi tangu miaka ya 1970, katika tasnia kilimo cha tumbaku.
Biashara yake ilivuka Rwanda na Burundi, alikuwa pia na shughuli za biashara katika nchi kama Uganda, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Angola, Sudan Kusini, Afrika Kusini na Nigeria.