YACHT YA KIFAHARI YAZAMA DAKIKA 15 BAADA YA SAFARI YAKE YA KWANZA

Yacht ya kifahari yenye thamani ya takribani dola 940,000 (sawa na shilingi bilioni 2.4 za Kitanzania) ilizama majini dakika 15 pekee baada ya kuanza safari yake ya kwanza, hali iliyowalazimu abiria na wahudumu wake kuruka majini kwa hofu.

Klipu ya video iliyopigwa na mashuhuda inaonyesha chombo hicho, kilichopewa jina Dolce Vento, kikizinduliwa kwenye maji katika mwambao wa Zonguldak, kaskazini mwa Uturuki, Jumanne, kabla ya kuanza kuyumba upande mmoja na hatimaye kuzama taratibu.

Ilikuwa mara ya kwanza yacht hiyo yenye urefu wa futi 85 kuzinduliwa baharini tangu kukabidhiwa kwa mmiliki wake kutoka Istanbul. Mmiliki, nahodha na wafanyakazi wawili waliruka baharini na kuogelea hadi ufukweni bila kupata majeraha. Walinzi wa Pwani na vikosi vya bandari waliwasili haraka na kuweka ulinzi kuzunguka chombo kilichokuwa kinazama.

Maafisa wa kiwanda kilichotengeneza yacht hiyo wamesema chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa, na ukaguzi wa kiufundi utafanyika ili kubaini kilichosababisha kuzama kwake.

Share: