Waziri ummy ataka ripoti ya kifo cha mjamzito na kichanga ndani ya siku  7

baada ya kupokea taarifa ya Uchunguzi, kila mtumishi aliyehusika atachukuliwa hatua kali za kitaaluma, kiutumishi na kijinai ikiwemo kufikishwa Mahakamani

Waziri wa Afya Mhe. Ummy mwalimu ametoa maelekezo kwa Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC) kuhakikisha ndani ya Siku 7 wamempelekea taarifa ya tukio la kifo cha mjamzito na kichanga chake kilichotokea tarehe 11 Novemba 2023 Mkoani Tanga. 

Amesema, tayari hatua za awali zimeshachukuliwa ikiwemo ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba kutuma timu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa inayojumuisha Madaktari bingwa wawili akiwemo Daktari Bingwa wa Wanawake na Uzazi na Daktari Bingwa wa Huduma za Usingizi ili kufanya uchunguzi wa tukio hili.

“Hatua nyingine iliyochukuliwa baada ya tukio hilo ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kuwasimamisha kazi watumishi watatu (3) walioshiriki kumpatia huduma mama huyo tangu alipopokelewa kituoni hadi umauti ulipomkuta ili kupisha uchunguzi wa tukio hili baya na lisilopaswa kuvumiliwa.” Amesema Waziri Ummy

Pia Waziri Ummy amewahakikishia Watanzania kuwa baada ya kupokea taarifa ya Uchunguzi, kila mtumishi aliyehusika atachukuliwa hatua kali za kitaaluma, kiutumishi na kijinai ikiwemo kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma za kijinai pale itakapothibitika.

Mwisho, Waziri Ummy anatoa pole kwa familia iliyoguswa na msiba huu na ameahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kusimamia ubora wa huduma za Afya ili kufikia matarajio ya wananchi wote.

Share: