Ujumbe huo umesema Mollel aliuawa mara tu baada ya kutekwa na kundi la Hamas mnamo tarehe 7 Oktoba 2023.
Serikali ya Tanzania imethibitisha kupokea taarifa kutoka serikali ya Israel kuhusu kifo cha mwanafunzi Joshua Mollel aliyekuwa anasoma nchini Israel na aliyetekwa nyara tarehe 7 Oktoba 2023 wakati kundi la Hamas liliposhambulia Israel.
Kupitia ujumbe wa X iliyojulikana kama Twitter hapo awali,Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania January Makamba amesema ameongea na baba ya marehemu Joshua, Mzee Mollel kuhusu ujumbe huo.
Ujumbe huo umesema Mollel aliuawa mara tu baada ya kutekwa na kundi la Hamas mnamo tarehe 7 Oktoba 2023.
Ujumbe huo umeongeza kusema;
'Tunaendelea na mpango wa awali wa kuwapeleka Mzee Mollel na mwanafamilia mwingine pamoja na Afisa wa Serikali nchini Israel, kuungana na Balozi wetu na maafisa waliopo huko, kukutana na kuzungumza na mamlaka za nchi hiyo ili kupata taarifa za ziada. Kwa ridhaa ya familia, na itakapobidi, tutatoa taarifa za ziada katika siku zijazo'
Joshua ni mwanafunzi wa pili kutoka Tanzania ambaye kifo chake kimethibitishwa kufuatia shambulio hilo la Hamas baada ya kile cha Clemence Mtenga ambaye pia alikuwa Israel kwa masomo ya Kilimo.
Bw Mtenga na Mollel walikuwa nchini Israel kama sehemu ya mpango wa masomo, na walifika mwezi mmoja tu kabla ya shambulio hilo. Mtenga Alizikwa tarehe 28 Novemba nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro, Kaskazini mwa Tanzania.
Katika chapisho la Facebook, mamlaka huko Kibbutz Nahal Oz zilisema mwili wa Bw Mollel ulikuwa unashikiliwa na Hamas.
Makumi ya wakaazi wa Kibbutz Nahal Oz walikuwa miongoni mwa watu 1,200 waliouawa na wapiganaji wa Hamas.
Tangu wakati huo, takriban watu 18,600 wameuawa katika operesheni ya Israel huko Gaza, Hamas inasema.