Ingawa kasi ya kimbunga hicho ilipungua ilipokaribia ufuo wa Tanzania, bado ilisababisha mvua kubwa na upepo mkali
Watu watatu wanafahamika kufariki dunia na wengine zaidi ya 100 wameokolewa, baada ya kimbunga Hidaya kilichopungua nguvu kutua Tanzania mwishoni mwa wiki.
Ingawa kasi ya kimbunga hicho ilipungua ilipokaribia ufuo wa Tanzania, bado ilisababisha mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa ya kusini mwa nchi hadi Jumamosi.
Zaidi ya mabaharia 20 kutoka Tanzania na Zanzibar walikuwa miongoni mwa waliookolewa, ripoti zinasema, baada ya boti zao kuserereka katika eneo la maji ya Kenya.
Hata hivyo baharia mmoja anasemekana kupoteza maisha kutokana na machafuko ya baharini. Watu wengine 80 waliookolewa walikuwa katika Kisiwa cha Kilwa nchini Tanzania.
Hitilafu kubwa ya umeme iliyosababishwa na kimbunga hicho ilikumba sehemu kubwa ya Tanzania siku ya Jumamosi.
Huduma za feri kati ya kitovu cha kibiashara cha Tanzania, Dar es Salaam, na Zanzibar pia zilisitishwa kwa sababu za kiusalama. Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha nyumba kadhaa zilizoharibiwa na upepo mkali na miti iliyoanguka katika kisiwa cha Mafia.
Nchi jirani ya Kenya iko katika hali ya tahadhari kufuatia uharibifu huo.