Watu wanne wanadaiwa kumuua Joyce na kukata sehemu zake za siri na kuzikausha

Upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili washtakiwa wanne wanaodaiwa kumuua Joyce Ludeheka kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kisha kukata sehemu yake ya siri na kuikausha, utaendelea kutoa ushahidi wake hii leo kwenye mahakama kuu, Masjala ndogo ya Geita

Jana upande huo wa Mashtaka umeieleza mahakama namna kaburi lilivyofukuliwa na kuchukua sampuli kwa ajili ya vipimo vya vinasaba.

Tayari mashahidi wanne wametoa ushahidi kwa kueleza namna sampuli zilivyochukuliwa hadi kusafirishwa kwenda ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.

Kesi hiyo ya mauaji namba 29820 ya mwaka 2024 inasikilizwa na hakimu mwenye mamlaka ya nyongeza Fredrick Lukuna.

Watuhumiwa kwenye kesi hiyo ni Mateso Joseph, Thereza Luhedeka, Dogani Budeba na Lucas Elias wakazi wa Mbogwe mkoani Geita ambao wanadaiwa kutenda tukio hilo Oktoba 11, 2024 katika Kijiji cha Ikobe wilayani Mbogwe mkoani Geita.

Washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Joyce Ludeheka ambaye ni mdogo wa Thereza Ludeheka waliokuwa na mgogoro wa ardhi.

Kwa mujibu wa mashtaka, sehemu ya siri inayodaiwa kukatwa kwa marehemu ilikutwa nyumbani kwa mshtakiwa wanne Lukas Elias.

Shahidi wa 10 katika kesi hiyo ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Kituo cha Polisi Masumbwe, Frank Fredrick ameileza mahakama namna walivyokwenda kufukua kaburi la Joyce Ludeheka na kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi.

Fredrick ameiambia mahakama kuwa wakiwa wameambatana na daktari, askari kwa kushirikiana na wananchi walifukua kaburi na kuutoa mwili wa Joyce kisha daktari akachukua sampulu kutoka kwenye mwili huo.

Shahidi huyo ameleza kuwa daktari alichukua sehemu za nywele, kipande cha nyama kutoka kwenye unyayo wa mguu na kipande cha nyama kutoka kwenye sehemu ya uke wa marehemu.

“Sampuli hizo tulizichukua kwa lengo la kwenda kufanya uchunguzi ili kujua uke uliokutwa kwa mmoja wa washtakiwa ni wa Joyce au la na baada ya kuchukua tulisaini fomu ya makabidhiano mimi na daktari aliyechukua sampuli,” amesema Fredrick.

Shahidi wa 11 ambaye ni daktari, John Masule naye aliieleza mahakama namna alivyochukua sampuli kwenye mwili wa marehemu na kuwakabidhi polisi kwa ajili ya kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi wa vina saba.

Share: