Wanigeria wawili washikiliwa nchini kenya kwa mauaji ya mwanafunzi rita waeni

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya yameitisha maandamano nchi nzima kuhusu viwango vya dhuluma dhidi ya wanawake

Wanaume wawili, ambao polisi wa Kenya wanasema ni raia wa Nigeria, wamekuwa washukiwa wa hivi punde zaidi kukamatwa kwa mauaji ya kikatili ya mwanafunzi.

Wamefika mahakamani lakini hawajafunguliwa mashtaka wala kutakiwa kutoa maoni yao.

Katika mauaji yaliyowakasirisha Wakenya wengi, mabaki ya Rita Waeni, 20, yaligunduliwa yakiwa yametupwa kwenye mifuko ya taka katika nyumba ya kukodisha ya muda mfupi katika mji mkuu, Nairobi, tarehe 14 Januari.

Lakini kichwa chake, pamoja na simu yake na vitu vingine vya kibinafsi, havikuwepo.

Mauaji hayo yamesababisha miito ya kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake.

Wakenya wanne pia wako kizuizini kuhusiana na mauaji hayo, pamoja na mtu mmoja ambaye alikuwa akisafiri kwa pasipoti ya Msumbiji na alikamatwa alipokuwa akijaribu kuondoka nchini.

Polisi wamewataja washukiwa wawili wapya wanaoshikiliwa kuwa ni William Ovie Opia na Johnbull Asbor.

Bw Opia alikuwa na pasipoti ya Nigeria iliyokwisha muda wake na Bw Asbor alipoteza pasipoti yake miaka miwili iliyopita, polisi walisema.

Jeshi la polisi lilikamata vitu kadhaa kutoka kwenye nyumba ya washukiwa hao, vikiwemo kisu cha bucha na shoka dogo vinavyoshukiwa kutumika katika mauaji na ukeketaji wa mwanafunzi huyo wa chuo kikuu.

Bw Opia aliwaambia wachunguzi kwamba alinunua shoka hilo mtandaoni kwa ajili ya kujilinda, gazetu la kibinafsi la Nation liliripoti.

Wanaume hao wawili walikamatwa katika eneo la Ndenderu, mji ulio umbali wa kilomita 20 kutoka Nairobi na karibu na bwawa ambapo polisi walipata kichwa kinachoshukiwa kuwa cha Bi Waeni, pamoja na simu yake na baadhi ya vitu vyake vilivyotoweka.

Familia ya Bi Waeni kufikia sasa haijaweza kutambua kichwa kilichopatikana.

Familia hiyo ilisema wiki jana kwamba waliohusika walidai fidia ya shilingi 500,000 za Kenya ($3,100; £2,400) ili kumwachilia Bi Waeni, hata baada ya kufariki.

Njia ya kutisha ambayo mwili wake ulitendewa imewashangaza watu, akiwemo mtaalamu mkuu wa serikali wa uchunguzi wa miili Johansen Oduor, ambaye alisema "hajawahi kukutana na tukio kama hilo" katika taaluma yake ya uchunguzi.

Makundi ya haki za binadamu na ya kutetea haki za wanawake yamepanga maandamano nchi nzima kupinga kile wanachokiona kuwa ongezeko la mauaji ya wanawake na unyanyasaji dhidi ya wanawake.

Kumekuwa na visa vya mauaji ya kikatili ya wanawake tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Utafiti nchini Kenya wa mwaka 2022 uligundua kuwa angalau 34% ya wanawake walisema waliwahi kufanyiwa ukatili wa kimwili wakati fulani maishani mwao.

Share: