Wanaume washtakiwa kuwaua ndege 3,600 wakiwemo tai

Wanaume wawili wa Marekani wameshtakiwa kwa kuwaua ndege wapatao 3,600 kinyume cha sheria, wakiwemo tai wenye vipara na wenye rangi ya dhahabu.

Simon Paul na Travis John Branson wanadaiwa kuwapiga risasi ndege hao kwa miaka kadhaa na kuuza sehemu na manyoya kwenye soko haramu.

Walishtakiwa kwa kula njama, kukiuka Sheria ya Ulinzi wa Tai na kufanya ulanguzi wa ndege hao kwa njia haramu.

Wanaume hao wawili waliamriwa kufika mahakamani mwezi Januari.

Mashtaka yaliyotolewa hadharani siku ya Jumatano yanadai kuwa waliwaua ndege kwenye Hifadhi ya Wahindi ya Flathead magharibi mwa Montana na kwingineko.

Shtaka lilisema Bw Branson alituma jumbe za kujisifu kuhusu "kufanya uhalifu" na "kutekeleza mauaji", na kwamba wawili hao waliuza ndege na manyoya yao kwa "kiasi kikubwa cha pesa".

Wakati fulani, wanaume hao waliweka mzoga wa kunguru ili kuvutia kundi la ndege kwenye eneo kabla ya kuwapiga risasi.

Hati ya mashtaka inaorodhesha matukio 13 tofauti ya madai ya ukiukaji wa Sheria ya Ulinzi wa Tai, lakini waendesha mashtaka hawakubainisha ni aina gani nyingine za ndege ambao wanaume waliua au ikiwa wengi walikuwa wachache au walikuwa hatarini.

Share: