Wanandoa Jijini Mbeya wakamatwa kwa mauaji ya mtoto wao

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni Ramadhan Tembo Mwakilasa (28) na Mariamu Charles Mwashambwa (28) wote wakazi wa TEKU viwandani jijini Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya mtoto Chloy Ramadhan (04) kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake.




Akizungumzia tukio hilo kamanda wa Polisi kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, ameeleza kuwa mnamo Novemba 25, 2024 majira ya saa mbili usiku ndipo wanandoa hao walimwadhibu mtoto huyo kwa kushirikiana hali iliyosababisha kifo chake baadaye.

Pamoja na kueleza hayo, amewataka wazazi na walezi kuishi vizuri na watoto badala ya kuchukua hatua zinazosababisha madhara.

"Ni kwamba huko katika mtaa wa TEKU viwandani Jijini Mbeya mtoto Chloy Ramadhan mwenye umri wa miaka minne alifariki Dunia baada ya kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi aitwaye Ramadhan Tembo Mwakilasa (28) akishirikiana na mama yake wa kambo aitwaye Mariamu Charles Mwashambwa (28). Uchunguzi umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ukatili na unyanyasaji kwa kumuadhibu mtoto baada ya kujisaidia kwenye nguo alizokuwa amezivaa kwahiyo jeshi la Polisi linawataka wazazi/walezi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watoto pindi wanapokosea na badala yake watumie njia sahihi na salama kuwafundisha au kuwaelekeza bila kusababisha madhara", ameeleza kamanda Kuzaga akitoa taarifa kwa wanahabari.

Share: