Wananchi Kahama watakiwa kuchangamkia fursa za miradi ya TACTIC

Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wamehimizwa kujiandaa kikamilifu kutumia vyema fursa mbalimbali zinazotokana na ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayotekelezwa kwenye Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, kupitia mradi wa uboreshaji Miji Tanzania (TACTIC) unaotekelezwa kwenye Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Kauli hiyo imetolewa wakati huu ambapo leo Jumatano Disemba 04, 2024 kumeshuhudiwa utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa kituo kikuu cha Mabasi eneo la Mbulu, Mkataba wa ujenzi wa Soko la Sango pamoja na ujenzi wa kituo kidogo cha Mabasi na soko la wajasiriamali eneo la Zongomera, miradi inayotarajiwa kukamilika Disemba 2025 na ikigharimu jumla ya shilingi Bilioni 20. 864.

Mhandisi Humphrey Kanyenye, Mratibu wa Miradi inayotekelezwa nchini Tanzania kwa ushirikiano kati ya Benki ya dunia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kupitia TARURA amesema kuboreshwa na kujengwa kwa miundombinu hiyo ina lengo la kuboresha utoaji wa huduma nchini na hivyo kusaidia wananchi na serikali kujipatia kipato kupitia miradi hiyo.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi hiyo inayotekelezwa Wilayani Kahama, Mhandisi Kanyenye amesema Katika soko la Zongomera matarajio ni kuongeza vizimba vya wafanyabiashara kutoka 58 hadi 200, kujenga migahawa ya Mamalishe na Babalishe 60 suala ambalo litaongeza mapato kutoka Milioni 11.760 hadi kufikia Milioni 31.2.



Aidha kwenye kituo kikuu cha Mabasi Mbulu, amesema matarajio ni kuweza kuhudumia wafanyabiasgara 700 kutoka 400 wa sasa, kuwa na vibanda vya wajasiriamali 204 kutoka 142 vya sasa pamoja na ujenzi wa kituo cha Polisi na hivyo kuongeza mapato kutoka Milioni 189 hadi kufikia milioni 470 za kitanzania.

Kadhalika akieleza kuhusu ujenzi wa Soko la Sambo, Mhandisi Kanyenye amesema soko hilo baada ya kukamilika ujenzi wake litakuwa na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara 802 kwa kuwa na vibanda 452 pamoja na vizimba 350 na hivyo kuongeza mapato kutoka sifuri hadi kufikia Shilingi Milioni 258.960.

Share: