Waliomuua rapa a.k.a wafikishwa mahakamani

Watuhumiwa watano kati ya wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya rapa wa Afrika Kusini, Kiernan Forbes, maarufu A.K.A, na rafiki yake wa karibu na mpishi maarufu nchini Afrika kusini Tebello "Tibz" Motshoane, wamefikishwa mahakamani mapema hii leo alhamisi.

Kesi hiyo, ambayo imerushwa moja kwa moja kwenye vituo kadhaa vya TV vya Afrika Kusini na kwenye mitandao ya kijamii, imeahirishwa hadi wiki ijayo.

Watano hao waliingia kizimbani kwa mara ya kwanza na kusimama wakitazama chini wakiwa wamefunika nyuso zao kabla ya mahakama kuamuru kuzivua kofia na mavazi waliyokuwa wametumia kufichia nyuso zao zisionekane.

Mwendesha mashtaka amewasomea mashitaka 10 yakiwamo ya mauaji, kula njama ya mauaji, kujaribu kuua na kumiliki silaha kinyume cha sheria.

AKA na Motshoane walipigwa risasi nje ya mkahawa mmoja katika mji wa pwani wa Durban mwaka mmoja uliopita mauaji ambayo yaliishangaza Afrika Kusini, ambayo ina viwango vya juu zaidi vya uhalifu duniani.

Share: