Wakazi wa kijijini mbezi beach b wagoma kuhama

Wakazi wa eneo la Kijijini lililopo katika Kata ya Kawe, Mtaa wa Mbezi Beach B, Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam wamekahidi kuhama eneo hilo kama ilivyoamuliwa na Serikali.

Wakazi hao walipewa siku 14 za kuhama eneo hilo kwa hiari na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Matambule.

Aidha, kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya kuaminika, inadaiwa kuwa, Jeshi la Polisi Wilaya ya Kinondoni, Maafisa kutoka TARURA na DAWASA Novemba 17, walifika katika eneo hilo na kukuta wakazi hao wakiwa hawajatekeleza agizo lililotolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, ambapo, Jeshi hilo liliwataka wakazi hao hadi kufika jana saa 5 asubuhi kuwa wameshahama.

Habari za ndani zinaeleza kwamba badala ya wakazi hao kuhama kwa hiari yao, wameamua kuagiza mganga wa kienyeji kutoka mkoani Mtwara ili awafanyie zindiko wasiweze kuondoka eneo hilo.

“Kinachoendelea kwa sasa ni wananchi hao kuanza kupimana ubavu na Serikali. Badala ya kuondoka sasa wamemuagiza mganga kutoka Mtwara ili awafanyie zindiko na wanadai kuwa huyo ni Mganga wao ambaye wamekuwa wakimtumia miaka yote,” alisema mtoa habari wetu.

Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mtambule, aliagiza wakazi hao kuhama eneo hilo kwa hiari ndani ya 14 kama walivyoomba, lakini hadi jana maisha yalikuwa yanaendelea kama kawaida.

Mwishoni mwa wiki Polisi walifika eneo hilo ambapo pamoja na mambo mengine walishuhudia wakazi hao wakiendelea kuishi kwenye vibanda, ambavyo wamekuwa wakitumia kufanya maovu.

Uamuzi wa Serikali kutaka wananchi hao kuhama eneo hilo unatokana na mtandao wa TimesMajira Online hivi karibuni kuibua maovu yanayofanyika katika eneo hilo dogo.

Katika eneo hilo, kuna kaya kati 30-40 ambazo zinaishi katika vibanda vya mabati, ambavyo ndiyo makazi yao ya kudumu kwa takriban miaka 30.

Makazi hayo huyatumia kama sehemu zao za kufanyia biashara haramu, ambazo wao wamezihalalisha. Biashara zinazofanyika katika eneo hilo ni uuzaji wa dawa za kulevya, bangi, pombe haramu ya gongo, pombe za kienyeji na ngono ya nipe nikupe (kununua).

Biashara ya ngono ya nipe nikupe katika eneo hilo, inahusisha wanawake na wasichana wenye umri mdogo. Kinachofanyika ni maelewano na baada ya hapo, maisha yanaendelea.

Wakati wakazi wanaoishi eneo la Kijijini wakiwa wameridhika na maisha ya eneo hilo, baadhi ya wananchi waliokuwa na nyumba za kudumu jirani ya Kijijini wamezikimbia na kwenda kuishi kwingineko, kwani eneo hilo sio salama kwa malezi ya watoto na kwenye suala zima la maadili.

Mbali na hilo, pia eneo hilo limeonekana kuwa ni hatarishi kwa watoto chini ya miaka 18. Mbali na lugha chafu zinazozungumzwa na wanaofika kupata huduma, lakini kibaya zaidi watu hao wamesahau kwamba kuna vyombo vya dola.

Baada ya Chanzo hicho kufika eneo hilo, lilishuhudia na kujiridhisha kufanyika kwa biashara haramu na kujionea jinsi watoto wanaoishi jirani wanavyokabiliwa na tishio kubwa la kimaadili.

Share: