Venezuela yamkabidhi bilionea fat leonard kwa serikali ya marekani

Bilionea maarufu aliyekuwa mafichoni akijulikana kama Fat Leonard amerejeshwa Marekani katika mpango wa kubadilishana wafungwa na Venezuela, Ikulu ya White House imethibitisha.

Mtoro huyo, ambaye jina lake halisi ni Leonard Glenn Francis, alipanga ulaghai wa $35m (£30m) dhidi ya Jeshi la Wanamaji la Marekani, Alitoroka kutoka kizuizini nchini Marekani mnamo 2022.

Raia kumi wa Marekani waliokuwa wakizuiliwa nchini Venezuela waliachiliwa huru kama sehemu ya makubaliano hayo.

Katika mpango huo wa kubadilishana wafungwa, Marekani ilimwachilia Alex Saab, msaidizi wa rais wa Venezuela.

Francis, mfungwa mashuhuri zaidi aliyehusishwa katika mpango huo, alizuiliwa Septemba 2022 akijaribu kupanda ndege kutoka Venezuela kuelekea Urusi wakati akikimbia kutoka kwa mamlaka ya Marekani.

Mfanyabiashara huyo wa Malaysia alitoroka kifungo cha nyumbani huko California wiki mbili zilizopita, alikokuwa akishikiliwa baada ya kukiri kuhusika katika kashfa iliyogharimu mamilioni ya dola za Marekani na kuhusisha makumi ya maafisa wa jeshi la wanamaji.

Waendesha mashtaka wanasema alitumia biashara yake ya Singapore  ambayo ilikuwa na kandarasi za kuhudumia meli za wanamaji za Marekani na kuwalaghai Jeshi la Wanamaji la Marekani, huku pia akiwapa maafisa wa Marekani pesa taslimu na zawadi kama rushwa.

Nyaraka za mahakama zilizowasilishwa kama sehemu ya makubaliano yake ya ombi zilimshutumu Francis kwa kuwapa maafisa wa Marekani zawadi za mamilioni ya dola, ambazo ni pamoja na safari za kifahari pombe za bei ghali, divai pamoja na huduma za ukahaba.

Share: