Utafiti ufanyike, vijana wanapenda utajiri bila kufanya kazi. Mch.Matonya

Utafiti ufanyike, vijana wanapenda utajiri bila kufanya kazi. Mch.Matonya

Kuelekea mwaka 2050, Serikali ya Tanzania imeshauriwa kuandaa na kufanya utafiti kujua kile kinachowasibu Vijana wa Kitanzania kutokana na Vijana wengi kutamani kuwa na maisha mazuri na kumiliki bidhaa na mali za gharama kubwa huku wakiwa hawana morali na motisha za kufanya kazi kwa bidii na kuthamini kazi na ajira wanazopewa kuzifanya.

Mchungaji Kanoni Moses Matonya, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania ametoa wito huo leo Jijini Dar Es salaam, wakati akitoa maoni yake kuhusu Rasimu ya pili ya Dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, akihimiza umuhimu wa kujenga Taifa la watu wenye moyo wa kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kufikia maendeleo binafsi na ya Taifa kwa ujumla.

Katika utafiti huo, Mchungaji Matonya amesema ndipo Taifa litakapobaini kinachosababisha Vijana kuchukia ajira na kazi sambamba na kuweza kutoa fursa ya kuandaliwa mkakati maalum wa kukuza bidii, ufanisi na kujituma kwa Vijana wa Kitanzania ambao wamekuwa na matamanio na ndoto za kuwa matajiri na wamiliki wa miradi, mitaji na mali mbalimbali bila ya kuwa na ari na bidii kama walivyo Vijana wa Mataifa mengine yaliyoendelea duniani.

Share: