ULEGA AWAKARIBISHA WANANCHI WA MIKOA YA GEITA NA KAGERA UFUNGUZI DARAJA LA KIGONGO - BUSISI

Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amemhakikishia Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita Fatma Mwassa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuwa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) umekamilika na kuwaalika kushiriki ufunguzi wake Juni 19, 2025 utakaofanyika Mkoani Mwanza.

Waziri Ulega amesema hayo leo Juni 10 2025, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ambapo amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo hivyo anawaalika wananchi wa Mikoa ya Geita na Kagera ambao ni wanufaika wakubwa wa Daraja hilo kushiriki kikamilifu.


"Dkt. Samia amekamilisha kazi hii kubwa ya kihistoria kwa Kanda ya Ziwa na taifa kwa ujumla hivyo jitokezeni kwa wingi katika ufunguzi huo", amesisitiza Ulega.


Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema wananchi wa mikoa hiyo ambao ndio wanufaika wakubwa wa Daraja hilo wamejipanga kujitokeza kikamilifu kwenye ufunguzi huo.

Aidha, Amempongeza Waziri Ulega kwa usimamizi mzuri wa miradi ya ujenzi inayoendelea katika Mikoa ya Geita na Kagera.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita, Bw. Nicholas Kasendamila amesema wananchi wa Geita wamejipanga kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi huo ili kutoa shukrani zao kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kuifungua mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.

Waziri Ulega yuko katika ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua miradi ya ujenzi inayoendelea.

Share: