Tope na takataka vyachangia daraja la jangwani kuziba nyakati za mvua

wakuu wa Mikoa na Wilaya watoke maofisini na kwenda kuangalia hali wanazopitia wananchi wao hasa kipindi hiki cha mvua nyingi na watatue kero zao wasishie tu kukaa maofisini

Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa OR-TAMISENI Mhe. Mohamed Mchengerwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Novemba 13, 2023 wamefika na kukagua athari za mvua katika daraja la Jangwani na kutoa kauli ya Serikali kuhusu hatua zinazofanyika sasa na zinazotarajiwa kufanyika ambazo ndio mwarobaini wa kuondoa kabisa kero zinazowakabili wananchi hasa nyakati za mvua.

Viongozi hao waliwasili katika eneo hilo nakujionea hali ya daraja lilivyo ambapo wameona tope  na takataka zikiwa zimezagaa chini ya daraja hilo na kuleta adha kwa wanaotumia daraja hilo, maji kushindwa kupita na kusababisha mafuriko hali inayowapatia ugumu wenye vyombo vya moto na wapita kwa miguu.

RC Chalamila alisema, "Sisi kama mkoa tuna wajibu wa kuangalia jambo lakufanya kila siku ya Mungu, jambo moja wapo ni kuhakikisha tunaendelea na uzibuaji wa daraja hili ili maji yaendelee kupita kirahisi."

Aidha Mhe Chalamila amesma kuna ulazima wa kuongeza kina na kutoa elimu ya mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na elimu ya usafi wa mazingira kwa jamii kutokana na utupaji ovyo wa takaka na machupa zinazotokana na shughuli za kibinadamu hali inayopelekea kuziba kwa daraja hilo.

Pia Mhe Chalamila alitoa rai kwa wananchi wanaoishi mabondeni wahame, "Viwanja ni kweli walinunua wao, nyumba walijenga wao na kuhama tunaomba na tuwashauri kwamba chukueni jukumu la kuondoka kama mnadhani maji yanaweza kuleta athari ila kwa wale wabishi mimi sina kipingamizi, utaishi na maji sawa, lakini kama utakufa utaleta hasara kwa taifa na familia yako," alisema RC Chalamila.

Naye Waziri wa Ujenzi Mhe. Bashungwa amemtaka meneja wa TANROAD Mkoa kuhakikisha takataka na tope lililojaa eneo la daraja linitolewa ili maji yaweze kupitana sio kusambaa na kupita juu ya daraja sambamba na hilo kugusia pia juu ya ubunifu wa daraja kubwa litakalokuwa suluhu ya muda mrefu. 

Vilevile Waziri wa TAMISENI Mhe. Mohamed Mchengerwa amehimiza na kuwataka wakuu wa Mikoa na Wilaya watoke maofisini na kwenda kuangalia hali wanazopitia wananchi wao hasa kipindi hiki cha mvua nyingi na watatue kero zao wasishie tu kukaa maofisini kusubiri kuletewa taarifa.

Share: