
Makamu wa Rais amesema Bara la Afrika ni muhimu kuweka kipaumbele kujenga uhimilivu katika mabadiliko ya tabianchi ambayo yatahitaji fedha za uhakika ili kuweza kuzuia na kukabiliana na hali hiyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inaendelea na dhamira ya kushiriki katika kutekeleza Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063 kupitia uwekezaji wa kimkakati katika sekta mbalimbali kama vile Miundombinu ya Usafirishaji, Nishati, Kilimo, Viwanda, TEHAMA, Uhifadhi wa Mazingira pamoja na maendeleo ya Rasilimali watu.
Makamu wa Rais amesema hayo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 42 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Bodi ya Juu ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA – NEPAD) uliyofanyika kwa njia ya Mtandao na kuongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo ambaye ni Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah El- Sisi.
Aidha Makamu wa Rais amesema ni muhimu nchi za Afrika kuimarisha vyanzo vya mapato vya ndani kwa kutumia vema rasilimali za nchi kama vile madini pamoja na kushirikiana na sekta binafsi ili kuweza kukabiliana na upungufu wa fedha za ufadhili wa miradi katika kutekeleza Ajenda 2063.
Pia Makamu wa Rais amesema ni muhimu kutumia fursa ya maendeleo kidijitali ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu ya kidijitali, kuwezesha biashara jumuishi ya mtandao pamoja na kuimarisha biashara za chini na biashara za kati.
Halikadhalika amesema kutokana na migorogoro na vita katika baadhi ya maeneo Barani Afrika, ni vema Mataifa ya Afrika kuungana pamoja katika kuhakikisha amani inapatikana ili Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063 iweze kufanikiwa.