Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mwaka 2015, Tanzania iliunga mkono Ajenda ya Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Afya na kuharakisha utekelezaji wa Sheria za Afya za Kimataifa ili kuzuia magonjwa ya kuambukiza kusambaa kimataifa.
Kupitia tathimini ya pamoja ya mwaka 2023 matokeo ya maendeleo ya Tanzania katika suala hilo inaonyesha hatua kubwa ambapo mwaka 2016 imedhihirika azma imara ya Serikali katika kutekeleza Sheria za Afya za Kimataifa kwa kutumia njia moja ikikubali uunganishaji wa afya ya binadamu, wanyama, na mazingira.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Novemba 13, 2024 katika ufunguzi wa Kongamano la 14 la Kimataifa la Sayansi la Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya (CUHAS) lililofanyika jijini Mwanza lenye kaulimbiu “Afya Moja na Usalama wa Afya wa Kimataifa”.
Ametaja jitihada zilizofanywa na Serikali za kuhuisha miongozo na mipango kazi ili kutekeleza Ajenda ya Mpango wa Kimataifa wa Usalama wa Afya.
“Mwongozo wa Kitaifa wa Maabara na Usalama wa Bioteknolojia, Ajenda ya Mpango ya Kazi wa Taifa wa Usalama wa Afya, Mpango wa Mkakati wa Afya Moja (2022-2027), Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa (UVIDA 2023-2028). Pamoja na kuhamasisha ukuzaji na uendelezaji wa raslimali watu na kuchochea ushirikiano wa kisekta,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendea kusema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kufanya jitihada za kuhakikisha Usalama wa Afya wa Kimataifa hasa kwa kutoa ufadhili wa masomo na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa lengo la kuongeza nguvu kazi kila mwaka.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inathamini mchango wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya pamoja na Kituo cha Tiba cha Bugando kwa ushirikiano na washirika wa ndani na kimataifa kwa kuwa mabingwa katika nyanja mbalimbali za utafiti zinazohusiana na Usalama wa Afya wa Kimataifa,” ameeleza Dkt. Biteko.