TANAPA kuingia kwenye biashara hewa ukaa

Shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA) liko kwenye utaratibu wa kuandaa mikataba ya makubaliano baina ya TANAPA na makampuni yanayohusika na biashara ya hewa ukaa ili liweze kunufaika na biashara ya hewa ukaa kama hifadhi za nchi nyingine zinavyonufaika na biashara hiyo.

Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula alipokuwa anajibu swali la Mhe. Zaytun Seif Swai aliyetaka kujua ni wakati gani TANAPA watatumia vizuri fursa za misitu waliyonayo ili tuweze kunufaika na biashara ya Carbon kama nchi nyingine zinavyofaidika.

Aidha Mhe. Kitandula alisema kuwa Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania iliwasiliana na Kituo cha Uratibu wa Biashara ya Hewa Ukaa cha Taifa (National Carbon Trade Centre) kilichopo katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) ili kupatiwa Mwongozo wa Biashara ya Hewa Ukaa (The National Carbon Trading Guideline) ulioandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Shirika limebainisha Hifadhi zenye fursa ya biashara hii katika maeneo ya kaboni ya kwenye udongo (Soil Carbon), Kaboni ya kwenye miti (Forest Carbon) na Kaboni ya kwenye maji (Blue Carbon)” alisema Mhe. Kitandula.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni miongoni mwa Taasisi za Serikali zenye maeneo ya misitu na linatambua uwepo wa biashara ya hewa ukaa yenye manufaa makubwa kwa kuchangia fedha za kigeni katika pato la taifa.

Share: