Ajali mbaya za boti ni za kawaida nchini DR Congo, ambapo boti mara nyingi hujaa abiria ambao ni nadra kupewa jaketi za usalama
Takriban watu 80 wamefariki dunia baada ya boti kuzama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, rais wa nchi hiyo amesema.
Maafa hayo yalitokea Jumatano kwenye Mto, kilomita 70 kutoka mji wa Mushie katika jimbo la Maï-Ndombe karibu na mpaka na nchi jirani ya Kongo-Brazzaville.
Katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii, Rais Félix Tshisekedi alisema "amehuzunishwa".
Rais alisema walioathiriwa watapata usaidizi na pia akaagiza uchunguzi ufanyike kubaini kilichosababisha.
"Rais wa Jamhuri anatoa wito wa uchunguzi kuhusu sababu za kweli za tukio hili la kusikitisha, ili kuzuia maafa kama haya kutokea tena katika siku zijazo," ofisi ya rais ilisema kwenye X, ambayo zamani ilikuwa Twitter.
Ajali mbaya za boti ni za kawaida nchini DR Congo, ambapo boti mara nyingi hujaa abiria ambao ni nadra kupewa jaketi za usalama na mara nyingi hawawezi kuogelea.