Takriban watu 11 wamefariki na wengine zaidi ya 60 hawajulikani walipo kutokana na ajali mbili za meli italia

Takriban watu 11 wamefariki na wengine zaidi ya 60 hawajulikani walipo kutokana na ajali mbili za meli katika pwani ya kusini mwa Italia, waokoaji wamesema.

Shirika la misaada la Ujerumani RESQSHIP limesema liliwachukua watu 51 kutoka kwenye mashua iliyozama, ya mbao na kupata miili 10 ikiwa imekwama karibu na kisiwa cha Lampedusa siku ya Jumatatu.


Katika tukio tofauti siku hiyo hiyo, zaidi ya watu 60 waliripotiwa kutoweka, huku 26 kati yao wakihofiwa kuwa watoto, shirika la Médecins Sans Frontières (MSF) lilisema.

Boti hizo zilikuwa zimebeba wahamiaji waliokuwa wametoka Libya na Uturuki, mashirika ya Umoja wa Mataifa yalisema.

Manusura wa ajali ya meli karibu na Lampedusa walikabidhiwa kwa walinzi wa pwani ya Italia na kupelekwa pwani siku ya Jumatatu asubuhi, wakati marehemu walikuwa wakivutwa hadi kisiwani, kulingana na RESQSHIP.


Boti hiyo ilikuwa imetoka Libya, na ilikuwa imebeba wahamiaji kutoka Syria, Misri, Pakistan na Bangladesh, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, yalisema katika taarifa ya pamoja.

Ajali nyingine ya meli ilikuwa karibu maili 125 kutoka pwani ya Calabria kusini mwa Italia, mashirika hayo yalisema.

Mmoja wa watu 12 walionusurika alikufa baada ya kuteremka, walinzi wa pwani wa Italia walisema.

Share: