Shirika la Kukabiliana na Majanga la Somalia (Sodma) linasema limekuwa likipokea simu za mara kwa mara kutoka kwa watu wanaoishi katika eneo la al-Shabab, lakini halina uwezo wa kusaidia kwani itakuwa hatari sana kwa maafisa kujitosa huko.
Maji yanayosonga kwa kasi yamesomba makaburi katikati mwa jiji la Galkayo nchini Somalia, na kuacha miili ikielea mitaani, kufuatia mafuriko mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika karne moja.
Kuonekana kwa miili iliyofukuliwa na mafuriko kumewatisha wakazi kama Ayaan Mohamed, anayeishi karibu na makaburi.
"Familia saba zikiwemo zangu zimeukimbia mtaa huo,"
"Mafuriko hayo yalifichua mabaki ya mwili wa Shekhe wa Kiislamu aliyeheshimika sana. Alizikwa miaka 18 iliyopita," Bi Mohamed anasema.
"Wanafunzi wake na mashekhe wengine walijaribu kukusanya mabaki," alisema, lakini hawakuweza kufanya hivyo.
Haya ni matukio ambayo jiji halijawahi kushuhudia hapo awali.
Takriban watu 32 wamefariki kote nchini humo, Umoja wa Mataifa unaonya kuwa zaidi ya watu milioni 1.6 wanaweza kuathiriwa na mafuriko makubwa ambayo yanakuja baada ya nchi hiyo kukumbwa na ukame wa miaka mingi.
Hali ya Galkayo si mbaya kama ilivyo katika eneo la Gedo kusini mwa Somalia, ambako Mto Juba umevnja kingo zake na kusomba daraja muhimu katika mji wa Bardere.
Maji yalizidi kimo cha daraja na likaporoma a siku ya Jumamosi.
Mohamed Abdirahin anasema takriban wakazi wote wa jiji hilo wamelazimika kuhamia viungani mwake.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 70 alikuwa mfanyabiashara na mkulima aliyefanikiwa hadi wiki iliyopita wakati mafuriko yalipoharibu mali zake.
"Niliacha kila kitu nyuma,"
"Niliokoa nilichoweza kwa mikono yangu kutoka kwenye duka langu – mali nyingine zilizobaki zilisombwa na maji. Ni kana kwamba maisha yangu yaliisha hivyo," Bw Abdirahin anasema.
Anapata ugumu wa kukubaliana na jinsi maisha yake yalivyobadilika haraka maji ya mafuriko yalipoingia dukani kwake kwanza, kisha kuangusha nyumba yake.
Bw Abdirahin pia alikuwa na shamba nje kidogo ya jiji, ambapo alienda kuangalia miti yake ya matunda iliyokomaa baada ya familia yake kulazimika kuondoka katika nyumba yao jijini.
Alikuwa akitarajia mavuno mengi mwishoni mwa mwezi wa Januari, lakini ndoto hiyo imetoweka.
"Miti ya maembe yenye urefu wa mita 10- (32ft-) ilikuwa karibu kuzama tulipokuwa tukiondoka, sikuweza kuona chochote kilichosimama kwenye ardhi yangu," Bw Abdirahin alisema.
Huku nyumba zikiwa zimezama kwa kiasi na mabaki ya binadamu yakielea karibu, wanahofia kuzuka kwa magonjwa, anasema.
Baadhi ya miili hiyo ilitambulika, na kuwatia kiwewe zaidi watu - na maji yanapopungua mifupa iliyofukuliwa pia huonekana.
Sehemu moja ya jiji, ambayo iko sehemu ya muinuko , lakini haiwezi kufikiwa kwa barabara baada ya daraja kuporomoka kutokana na mafuriko.
Ni njia muhimu ya maisha kwa wale wote waliopoteza makazi yao kwani wilaya ina maduka ya chakula na kituo cha afya, Watu hutumia boti ndogo ili kufika huko.
"Tunasubiri zaidi ya saa nne kwa boti hizo kwenda kutuletea chakula," Bw Abdirahin alisema.
Serikali dhaifu ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imekuwa ikijaribu kutoa msaada wa dharura, lakini inasema haiwezi kushughulikia maeneo yote yaliyoathirika.
"Kwa siku tano zilizopita, tumetoa misaada mingi kwa wale wanaohitaji - hali ya sasa imezidi uwezo wa serikali," Naibu Waziri Mkuu wa Somalia Salah Jama.
Tatizo jingine ni kwamba baadhi ya maeneo hayako mikononi mwa serikali na yanadhibitiwa na kundi lenye mafungamano na al-Qaeda la al-Shabab.
Shirika la Kukabiliana na Majanga la Somalia (Sodma) linasema limekuwa likipokea simu za mara kwa mara kutoka kwa watu wanaoishi katika eneo la al-Shabab, lakini halina uwezo wa kusaidia kwani itakuwa hatari sana kwa maafisa kujitosa huko.
Katika baadhi ya miji watu ambao nyumba zao bado zimesimama wameambiwa kuwakaribisha wale ambao wameachwa bila makazi - na baadhi ya jamii zimekuwa zikikusanyika pamoja kupika chakula kwa ajili ya wenzao.
Wakati msimu wa mvua uliosubiriwa kwa muda mrefu unapofika nchini Somalia - kwa kawaida huwa ni wakati wa kusherehekea, kuashiria ustawi ujao, hasa wakati nchi hiyo imekuwa ikikumbwa na ukame.
Mara nyingi watu hujitosa nje kuchunguza mabwawa na mashimo ya kumwagilia ambayo hujaa na wakati mwingine kwenda kuogelea.
Mpwa na bintiye Anab Deerow, anayeishi El-Wak magharibi mwa Bardere kwenye mpaka na Kenya, alitoka kwenda kuburudika baada ya mvua kubwa kunyesha.
Bi Deerow alisema wasichana hao wawili walikuwa wamechangamka sana kwani walikuwa wamemaliza mitihani yao na ilikuwa siku ya kwanza ya likizo yao kabla ya kuanza shule ya sekondari mwaka ujao.
Binamu hao walikuwa wakicheza nje kwa saa chache, wakijipiga picha za selfie na walikuwa wameshuka tu chini kuona kidimbwi cha maji kwenye bonde dogo nje ya mji wakati waliposombwa na maji.
Binti ya Bi Deerow mwenye umri wa miaka minane alishuhudia na akaja akipiga kelele nyumbani kumwambia. Miili ya wasichana hao ilipatikana baadaye kufuatia msako wa muda mrefu baada ya maji kupungua.
"Walikuwa wamerejea kutoka shuleni siku moja kabla ya kufa. Sina neno. Inaonekana malaika wa kifo aliwaita," Bi Deerow.
Mvua kubwa na mafuriko yanatarajiwa kuendelea hadi mwisho wa Novemba, kulingana na Sodma.
Pamoja na wale ambao wamelazimika kuyahama makazi yao, mashamba yenye ukubwa wa heka milioni 1.5 yanaweza kuharibiwa na mafuriko Umoja wa Mataifa unaonya.
Wazo la mvua nyingi kunyesha linatisha kwa watu wengi ambao tayari wanatatizika kupata chakula na maji safi.
Bw Abdirahin na familia yake ya watu 12 sasa wamejikuta wakilala katika msitu mnene nje ya Bardere, ambako wamekuwa kwa zaidi ya wiki moja.
"Tumepotea vichakani kabisa," alisema huku akizidiwa na hisia.
"Tuko hai tu bila sababu. Tunaogopa. Tunasubiri tu msaada kutoka kwa Mungu."