Shambulizi baya la makombora lakumba soko la omdurman sudan

Zaidi ya watu 20 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya makombora kugonga soko katika kitongoji cha mji mkuu wa Sudan Khartoum, kundi la wanasheria lilisema.

Soko lililojaa watu huko Omdurman lilishambiliwa baada ya majibizano makali ya risasi kati ya jeshi la Sudan na Jeshi la Rapid Support Forces (RSF), Wanasheria wa Dharura wa Sudan, kundi lisilo la kiserikali lilisema katika taarifa siku ya Jumapili.

Chanzo cha matibabu kililiambia shirika la habari la AFP kwamba shambulizi hilo liliua watu 15 katika kitongoji cha Al-Thawra cha Omdurman.

Mawakili hao wamelaani pande hizo mbili zinazozozana kwa kuendelea na mapigano katika maeneo yenye watu wengi na kutaka kusitishwa kwa vita.

Mapigano hayo yanaendelea katika mji mkuu na katika miji mingine ya Darfur na eneo la Kordofan, huku kukiwa na mazungumzo kati ya vikosi hasimu huko Jeddah, Saudi Arabia.

Zaidi ya watu 9,000 wameuawa na wengine karibu milioni sita wametoroka makazi yao tangu mapigano yalipoanza katikati ya mwezi Aprili.

Share: