RC Makonda ataka kasi zaidi mradi wa ujenzi jengo la utawala jiji la Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda leo Alhamisi Januari 09, 2025, amekagua maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Jiji la Arusha na kuagiza mkandarasi anayesimamia Ujenzi huo kwa awamu ya pili (Phase 2) kuhakikisha kuwa anakamilisha kazi yake mwezi Mei mwaka huu badala ya mwezi Julai iliyokuwa imepangwa awali.

Mhe. Makonda amefikia uamuzi huo baada ya kuelezwa kuwa mradi huo umekuwa ukisuasua bila sababu za msingi ilihali tayari Rais Samia Suluhu Hassan alikwisha idhinisha zaidi ya Bilioni 6 za ujenzi wa awamu ya pili ya Jengo hilo la Ghorofa sita, Akitaka pia taratibu za kimkataba na Ujenzi kwa awamu ya tatu kuanza kuandaliwa haraka badala ya kusubiri kukamilika kwa ujenzi awamu ya pili.

Katika Hatua nyingine Mhe. Makonda pia amesisitiza Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kutumia wenyeji wa Arusha na wenye sifa kwenye tenda mbalimbali ili kukuza pato la Mkoa pamoja na kuwataka Madiwani, Wataalamu na Viongozi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha kushikamana na kuhakikisha kila wanachokifanya kinakuwa na matokeo chanya kwa Wananchi kama sehemu ya Kumpa sifa na Shukrani Rais Samia Suluhu Hassan anayehakikisha mara zote kuwa serikali yake haiwi kikwazo kwa maendeleo na ustawi wa wananchi wake.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maximilian Iranghe na Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Felician Mtahengerwa, wamemshukuru Mhe. Makonda kwa namna anavyokuza uwajibikaji Mkoani Arusha, wakiahidi kushirikiana na Wataalamu na Watendaji wengine katika kusimamia kikamilifu maelekezo ya Mhe. Paul Christian Makonda ili kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na Ujenzi wa Jengo hilo haraka iwezekanavyo.


Share: