Sabina amesema mahusiano yao yalianza kuwa na migogoro baada ya kulazimishwa na aliyekuwa Mume wake kuchukua mikopo benki

Mwalimu Sabina John Mosi mkazi wa Sakina Mkoani Arusha amemshukuru Mhe. Paul Christian Makonda Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kumfuta machozi yake ya miaka mitano baada ya kudhulumiwa magari yake na aliyekuwa Mume wake Ndugu Julius Mwase.

Mwalimu Sabina ametoa kauli hiyo leo Mei 09, 2024 wakati alipokuwa akizungumza na Wanahabari ikiwa ni siku ya pili ya Kliniki ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika kusikiliza na kutatua kero za Wananchi wa Arusha.

Sabina amesema mahusiano yao yalianza kuwa na migogoro baada ya kulazimishwa na aliyekuwa Mume wake kuchukua mikopo benki na baada ya kuchukua mkopo wa Milioni 250, mume wake alianzisha mahusiano na mwanamke mwingine, akianza pia kukumbatana na ukatili wa kijinsia na vipigo kutoka kwa aliyekuwa mume wake.

Jana Mei 08, 2024 Sabina alikuwa miongoni mwa wananchi waliofika kwenye viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kuwasilisha kero yake hiyo ambapo Mhe. Mkuu wa mkoa alimsikiliza na kuahidi kusimamia suala lake ili apate haki yake.

Leo alhamisi Jeshi la Polisi limefika eneo la Kwa Mrombo Murieti na kushikilia magari mawili yanayomilikiwa na Sabina na aliyekuwa Mume wake. Sabina alimueleza Mhe. Mkuu wa Mkoa Paul Christian Makonda kuwa magari hayo yamekuwa yakikatwa na kuuzwa kama spea na vyuma chakavu baada ya Aliyekuwa mume wake kushindwa kuyauza magari hayo kutokana na hati ya umiliki, kumilikiwa na wanandoa hao wa zamani na maadui wakubwa wa sasa.

Share: