Rc chalamila atembelea mto kinyerezi akuta hali si shwari atoa maagizo

shida wanazopata kwa kipindi cha mvua kutokana na mto huo unavyozidi kuwagawa wananchi wa mtaa huo na kukosa mawasiliano

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaa Mhe. Albert Chalamila Novemba 2, 2023 alifika katika mtaa wa Kinyerezi Kanga kujionea jinsi wananchi wa mtaa huo wanavyopata tabu ya kuvuka katika mto huo kwa kipindi cha mvua. 

RC Chalamila alisikiliza kero za wananchi hao na amewataka Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam, Wakala wa Barabara za mijini na vijijini (TARURA), Shirika la Maendeleo la Mafuta na Gesi (TPDC) kuangalia kibali kilichotolewa na Tanesco kuanza mchakato wa kujenga kivuko hicho mara moja Jumatatu ijayo

Aida Mhe. Chalamila amewataka kubuni kivuko ambacho hakina gharama kubwa sana, “Mimi nipo tayari kuidhinisha fedha kwa Mkurugenzi wa jiji ambaye pale tunakusanya fedha nyingi, mheshimiwa raisi anataka fedha hizo zitumike kwa watanzania,” alisema RC.

Pia aliwataka watu wa mipango miji wajithibitishie kwamba ni kweli hakuna barabara nyingine kama wananchi wa hapo walivyoeleza, na waliwezaje kujenga makazi katika eneo hilo.

Naye Diwani wa Kata ya Kinyerezi Bi. Leah Benardi alimshukuru RC kwa kufika pale na kujionea shida wanazopata kwa kipindi cha mvua kutokana na mto huo unavyozidi kuwagawa wananchi wa mtaa huo na kukosa mawasiliano na huduma za kijamii kwa pande hizo, ambao mwanzo mto huo ulikuwa mdogo ila kwasasa unazidi kuwa mkubwa kadri mvua zinapoendelea kunyesha.

Diwani Leah alisema mpaka sasa wana kamati ya kujenga kivuko kwa kujiongeza angalau kupata nguzo hivyo alimuomba mkuu wa mkoa usaidizi sababu hilo tatizo ni la muda mrefu.

Rukia Mwaita naye ni mwanafunzi wa darasa la sita anayeishi ng’ambo ya pili ya mto Kinyerezi alimweleza RC Chalamila shida wanazopata wakiwa wanaenda na kurudi shule wakisaidiwa kubebwa mgongoni na wavushaji wa eneo hilo huku wengine wakiwatoza pesa kwa huduma hiyo.

Share: