Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini kuanzia leo October 30 hadi 01 November 2023 ambapo mbali na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Tanzania na Ujerumani, Rais huyo anatarajiwa kuonana na kuzungumza na Vijana Wajasiriamali wa Kitanzania wanaojihusisha na uvumbuzi wa teknolojia mpya hususani matumizi ya akili bandia.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeeleza kuwa akiwa nchini, Rais Steinmeier atafanya mazungumzo rasmi na Mwenyeji wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam, October 31, 2023 na baada ya mazungumzo hayo, Viongozi hao watapata fursa ya kuongea na Waandishi wa Habari kuelezea kuhusu masuala muhimu yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo yao kesho hiyohiyo Rais Steinmeier anatarajiwa kuonana na kuzungumza na vijana Wajasiriamali wa Kitanzania wanaojihusisha na uvumbuzi wa teknolojia mpya hususan matumizi ya akili bandia ambao wanafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani.
Siku ya tarehe 01 Novemba 2023, Rais Stenmeier atasafiri kwenda Wilayani Songea Mkoani Ruvuma kutembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji na Shule ya Msingi ya Majimaji, hii ni makumbusho pekee nchini Tanzania inayoonesha historia kubwa ya Vita vya Majimaji katika harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.